Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limefanikisha kufungwa kwa mtambo unaoondoa ganda laini la korosho ili kuongeza thamani zao hilo kabla ya kusafirishwa.

Akizungumza leo Machi 29,2024 wakati wa kusaini makubaliano na makabidhiano ya mtambo huo kwa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (Camartec), Mkurugenzi Mkuu wa Tirdo, Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema lengo ni kuongeza thamani zao hilo kabla ya kusafirishwa.

Amesema walipewa jukumu la kuleta mitambo itakayoondoa ganda laini la korosho kukamilisha mnyororo mzima wa ubanguaji korosho.

Taasisi zingine zilizofanikisha kufungwa kwa mtambo huo ni Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (Temdo) na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (Sido). 

"Tunaishukuru serikali kwa kuziwezesha taasisi zetu kifedha na kuweza kupata mitambo kama hii," amesema Profesa Mtambo.

Kwa upande wake Mhandisi Atupele Kilindu kutoka Idara ya Uhandisi Maendeleo Tirdo, amesema mtambo huo uliogharimu Sh milioni 40 una uwezo wa kuondoa ganda laini kilo 350 kwa saa.

Amesema lengo ni kuanzisha kiwanda cha mfano kwa ajili ya kufundisha wajasiriamali namna ya ubanguaji na kuongeza mnyororo wa thamani katika zao la korosho.

Kaimu Mkurugenzi wa Camartec, Mhandisi Paythias Ntella, amesema tayari wana kiwanda darasa cha kubangua korosho kilichoanzishwa na kituo hicho wilayani Manyoni mkoani Singida.

Amesema kiwanda hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wakulima kubangua korosho na kuacha kuuza zikiwa ghafi na kushindwa kunufaika na kilimo hicho.

"Tunafundisha wajasiriamali katika hatua zote ili kubangua na kumenya ili vitengenezwe viwanda vingi zaidi sehemu nyingine," amesema Ntella.

Lengo la Serikali kuhakikisha asilimia 60 ya korosho zote zinazozalishwa nchini zinabanguliwa ifikapo msimu wa mwaka 2025/26 na asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.











KAMPUNI ya Mafuta ya Puma Tanzania imewakutanisha wadau mbalimbali katika Iftar iliyoandaliwa na Kampuni hiyo huku ikitumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania kuendelea kuwaunga mkono sambamba na kuhimiza kudumisha amani.

Hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Kampuni hiyo ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wake Fatma Abdallah imefanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa taasisi za umma na binafsi pamoja na wateja wa kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mgeni rasmi katika Iftar hiyo alikuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Walid aliyewakilishwa na Sheikh wa Wilaya ya Temeke ...

Akizungumza wakati wa Iftar hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni hiyo Dk Selemani Majige ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa ni vema kila Mtanzania kwa nafasi yake kuendelea kuliombea Taifa sambamba na kumuunga mkono Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

"Tunafahamu kwa sasa tunaendelea na Mfungo wa Ramadhan pamoja na Kwaresima hivyo wakati tukiendelea na Mfungo ni vema tukaliombea Taifa letu lakini wakati huo huo kudumisha Umoja,amani na mshikamano,"amesema Dk Majige.

Amesisitiza kuendelea kudumisha amani katika nchini Kunafanya uchumi Wetu kuendelea kuimarika na biashara zetu ziendelee vizuri."Kulinda amani ni jambo kubwa kwani kama hakuna amani basi hata biashara haziwezi kufanyika vizuri.

"Hivyo kupitia mwezi mtukufu wa Ramadhan ni vema kuendelea kumuomba Mungu na kuendelea kumuombea Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ili aendelee kutuongoza na kudumisha amani katika taifa letu."

Pia amewaomba Watanzania kuendelea kutumia mafuta ya Puma Energy Tanzania pamoja na bidhaa zake zote huku akifafanua mafuta ya Kampuni hiyo yana ubora na viwango vya hali ya juu.

"Tunawaomba muendelee kutumia mafuta ya Puma ili tuongeze faida na tukiongeza faida Serikali inapata gawio na inapotoa gawio zinapatikana fedha ambazo zinakwenda kuhudumia jamii katika maeneo mbalimbali,"

Kwa upande wake Sheikh wa Wilaya ya Temeke Sheikh Zailai Hassan Mkoyogole aliyemwakilishwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Walid Alhad Omar aliyekuwa mgeni rasmi, amesema kipindi hiki cha Mwezi mtukufu wa Ramadhan jambo kubwa ni kuzidisha wema kwa maana wanadamu ni wakosaji mbele za Mwenyezi Mungu.

"Binadamu anamkosea Mwenyezi Mungu kwa vitu vingi hivyo sasa ameleta Mwezi mtukufu wa Ramadhan ili kutubu kwa yale yote ambayo ameyafanya.Hivyo kinachotakiwa katika mwezi huu ni kufanya yale yaliyomema na kurejea kwake,"

Pia amesema Mwenye Mungu anapenda kuombwa ,hivyo ametoa mwito kwa watu wote kurejea kwa Muumba kuomba msamaha.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania Fatma Abdallah amewashukuru wadau waliojitokeza katika futari hiyo huku akitumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania kuwaunga mkono kwa kununua bidhaa za mafuta ya Kampuni hiyo.

Aidha amesema wao kama Puma Energy Tanzania wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali hasa katika kutekeleza matumizi ya nishati safi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kuendelea kutunza mazingira .

"Puma Energy Tanzania tunatambua mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na hasa kwenye suala la nishati safi hivyo tutaendelea kuaidia kwa lengo la kuhakikisha mazingira yanalindwa na matumizi ya nishati safi kwa watanzania yanakuwa kipaumbele."

Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu UDA- RT Waziri Kindamba aliyeshiriki futari hiyo amewapongeza kwa kuandaa futari hiyo ni kuwaalika wateja wao ambao wanatumia vilainishi na mafuta.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania Dk . Selemani Majige akisalimiana na Mkurugenzi wa UDA-RT Waziri Kindamba pamoja na wageni wengine waalikwa waliohudhuria futari iliyoandaliwa na Kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania Fatma Abdallah akisalimiana na wageni waalikwa wakati wa hafla ya Iftar iliyofanyikaa jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania Fatma Abdallah akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya Iftar iliyofanyikaa jijini Dar es Salaam












Na Mwandishi wetu- Dodoma

Serikali kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu inaendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na Madhara ya El Nino kuanzia Septemba 2023 hadi Juni 2024.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa-Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU) Brigedia Hosea Ndagala katika Kikao Kazi cha kujadili utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na Madhara ya El Nino Septemba 2023 hadi Juni 2024 ambapo alisema kutokea kwa maafa husababisha madhara ambayo huathiri utendaji kazi, kuzorotesha maendeleo na ukuaji wa kiuchumi kwa wananchi na kupotea kwa mafanikio yaliyopatikana kwa muda mrefu na hivyo, kuzorotesha hatua za maendeleo.

Alisema Maafa hayo yamekuwa yakisabibisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu na uharibifu wa mali na miundombinu, na ongezeko la tegemezi kutokana na Watoto kupoteza wazazi.

“Nchi yetu imekuwa ikishuhudia matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababisha maafa na kuathiri mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii. Maafa haya yamekuwa yakisabibisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu na uharibifu wa mali na miundombinu,”Alisema Brigedia huyo.

Aidha Brigedia Ndagala alizitaka kila sekta kuwasilisha tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na Madhara ya El Nino ambao una lengo la kuhakikisha serikali na wadau wanachukua hatua stahiki kuzuia au kupunguza madhara na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kutokana na maafa yanayosababishwa na El Nino ili kuokoa maisha na mali.

“Hatua hii ni muhimu ili kuweka mikakati ya pamoja kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa mvua za Masika. Ni imani yangu kuwa kikao kazi hiki kitatoka na mikakati madhubuti itakayosaidia kuendelea kuongeza ufanisi katika kukabiliana na maafa,” Alieleza.
 

Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Brigedi Hosea Ndagala akizungumza wakati akifungua Kikao Kazi Cha Kujadili Utekelezaji Wa Mpango Wa Taifa Wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na madhara ya mvua za El Nino kikao kilichofanyika Jijini Dodoma.
 

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Luteni Kanali Selestine Masalamado akichangia wakati wa wasilisho la Madhara yaliyotokana na mvua za El-Nino katika kikao kazi kilichofanyika Jijini Dodoma.
 

Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi wa Ubora wa huduma za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Bw. Geofrid Chikojo akitoa wasilisho kuhusu taarifa ya muelekeo wa mvua za msimu wa masika kwa mwezi Machi hadi Mei 2024 katika kikao kazi kilichofanyika Jijini Dodoma.
 

Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Morogoro Ndug. Anza-Amen Ndossa akichangia mada wakati wa wasilisho lililohusu madhara yaliyotokana na mvua za El-Nino katika kikao kazi kilichofanyika Jijini Dodoma .
 

Picha ya pamoja ya washiriki wa kikao kazi cha Kujadili Utekelezaji Wa Mpango Wa Taifa Wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na madhara ya mvua za El Nino katika kikao kazi kilichofanyika Jijini Dodoma.

 

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani Machi 29

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, anatarajia kuzindua rasmi kitabu chake ambacho kinahusu masuala mazima ya maadili, kitabia ndani ya jamii hususan kwa kundi la vijana, ifikapo mfungo mosi.

Aidha amewaasa watanzania kujenga tabia ya kusaidia makundi maalum pamoja na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu (yatima) kwa nyakati zote isiishie mwezi mtukufu wa Ramadan pekee.

Sheikh Zubeir alisema hayo katika iftari iliyoandaliwa na Rais dkt Samia Suluhu Hassan na kusimamiwa na Serikali mkoa wa Pwani, ambapo watu 500 wakiwemo watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu 300 ,wazazi wao , viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa , Taasisi na waalikwa wengine walijumuika katika futari hiyo.

Alieleza ,suala la maadili ni pana hivyo ni lazima kushirikiana ili kuwa na kizazi chenye maadili mema.

Sheikh Zubeir alitoa rai kwa jamii hususan kundi la vijana kutengeneza misimamo katika maadili na tabia njema ,ili kuwa na Taifa lenye maadili na mfano wa kuigwa Duniani.

"Ili Taifa lisimame vizuri na kuwa Taifa bora lazima kuwa na maadili kwani Hakuna Taifa bora ambalo linasimama pasipo watu wake kuwa na maadili bora" alisisitiza.

Vilevile alieleza kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaj Abubakar Kunenge kufuturisha futari kwa kula pamoja na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu ni jambo jema lakuigwa.

"Watoto hawa wanahitaji faraja ,wasiojiweza wasaidie na isiwe mwezi mtukufu wa Ramadan hata nyakati nyingine ,na tukijenga tabia hii ya kusaidia tutajikuta tunafikia kundi kubwa" aliongeza Sheikh Zubeir.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaj Abubakar Kunenge alieleza, mwaka 2023 alitoa futari Mkoani Pwani, Machi 27  Dodoma na Machi 28 mwaka huu mkoa umesimamia watu 500 Kati yao watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu 300 wamejumuika kufuturu .

Kunenge alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujali makundi maalum.

Mkuu huyo wa mkoa, aliziasa Taasisi zinazojihusisha kulea watoto ambazo zinakwenda kinyume na mikataba kwa kujinufaisha matumbo yao waache mara moja ,na wanachotakiwa ni kutekeleza malengo yao kwa watoto hao.

Nae Sheikh wa Mkoa wa Pwani, Khamis Mtupa
alisema waumini wa kiislam waendeleze kufanya yaliyo mema katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadan.

Alieleza,kutoa ni imani Hata kama ni kidogo na kwa kutambua hilo Wana kamati maalum ambayo wanafikia wasiojiweza, gerezani ,mashuleni ili nao waweze kupata futari.

Mtupa aliomba watanzania kuendelea kuliombea Taifa Amani na kumuombea Rais dkt Samia kufanya majukumu yake kwa afya bora.






 

 

Dar es Salaam Ijumaa 29 Marchi 2024 BancABC Tanzania, ambayo ni kampuni tanzu ya Atlas Mara imetoa msaada wa vyakula mbali mbali pamoja na kuandaa futari kwa watoto wanaolelewa kwenye kituo cha watoto yatima cha New Faraja kilicho Mburahati Jijini Dar es Salaam ikiwa ni ishara ya kuonyesha upendo kwenye kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadan.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam mara ya kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Idara ya Udhibiti BancABC Tanzania Saleh Geva alisema benki hiyo imetoa msaada pamoja na kufuturisha kituo cha Watoto yatima cha New Faraja kama ishara ya kuonyesha upendo pamoja na kuwapa tabasamu na hasa kwenye kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadan. 

‘Watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu wanahitaji kuonyesha upendo. Sisi BancABC Tanzania na hasa wafanyakazi tumefarajika sana kujumuika nao pamoja na kupata wasaa wa kufuturu na watoto wanaolelewa kwenye kituo hiki. Kilikuwa ni kipindi faraja sana kwao lakini furaha kwetu kuona watoto hawa wakitabasamu. Lengo letu ilikuwa ni kufanikiwa kuona watoto hawa wajisikia kama sehemu ya Jamii ya Watanzania’, alisema Geva.

Geva aliongeza ‘Kuwafanya watoto hawa watabasamu na kufurai kunawapa matumaini yao ya maisha ya baadae. Kuja kwetu kufuturu na watoto hawa kumetuonyesha kwa nini BancABC Tanzania imekuwa ikijikita sana kwenye kusaidia Jamii ambayo inayotuzunguka. Tutaendelea na utamanduni huu wa kusaidia Jamii ambayo inaishi kwenye mazingira mangumu kwa sababu tunaamini ni moja Kati ya nguzo ya sisi kuendelea kukua kibiashara’,

‘Furaha yetu sisi BancABC Tanzania ni kuona tukibadilisha maisha ya Watanzania. Tunaamini kwenye Jamii yenye usawa na ndio sababu mwaka huu tuliamua kuja kufuturu na watoto hawa ambao wanaishi kwenye mazingira magumu ’, alisema Geva.

‘BancABC Tanzania, ikiwa ni taasisi ya kutoa huduma za kifedha imekuwa ikifanya kazi kubwa sana kuwafikia Watanzania na hasa wale ambao bado hawafikiwa na huduma za kibenki. Kwa sasa, BancABC Tanzania tunao mawakala zaidi ya 700 nchini kote’, alisema Geva huku akiongeza kuwa benki hiyo inayo akaunti maalum kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wa kati kwa ajili ya kutoa mikopo ya kuimarisha biashara zao’.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo cha New Faraja Zamda Idrisa alisema kuwa wamefarijika kwa kuona taasisi binafsi kama BancABC Tanzania ikiunga mkono Jamii ambayo inaishi kwenye mazingira mangumu.

Aliongeza ‘Msaada wenu umekuja kwenye muda muafaka kwani watoto hawa wanahitaji kuonyesha upendo kama watoto wengine. Tunawashukuru kwa msaada wenu na tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kuwafungulia riziki kwenye maisha yenu ya kila siku’.

‘Tunatoa rai kwa taasisi zingine pamoja na watu binafsi wazidi kutusaidia kwani watoto hawa wanahitaji kuvaa, kusoma, chakula pamoja na matibabu na kituo chetu hakina wadhamini bali tunatengemea misaada kutoka kwa wadau mbali mbali kama BancABC Tanzania walivyokuja hapa kutusaidia kwa siku ya leo.


Mkuu wa Kitengo cha Idara ya Udhibiti BancABC Tanzania Saleh Geva akiwahudumia futari watoto wanaolelewa kwenye Kituo cha Watoto yatima cha New Faraja kilichopo Mburahati Jijini Dar es Salaam. BancABC Tanzania ambayo ni kampuni tanzu ya Atlas Mara ilitoa msaada wa vyakula mbalimbali pamoja na kuandaa futari kwa watoto waliopo kwenye kituo hicho kama ishara ya kuonyesha upendo kwenye kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadan.
Baadhi ya watoto wanaolelewa kwenye kituo cha watoto yatima cha New Faraja kilichopo Mburahati Jijini Dar es Salaam wakifuatilia hotuba pamoja na nasaha kutoka kwa viongozi wa BancABC Tanzania mara baada ya benki hiyo kutoa msaada wa vyakula mbali mbali pamoja na kuwaandalia futari watoto hao ikiwa ni ishara ya kuonyesha upendo kwenye kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadan.


Mkuu wa kitengo cha Udhibiti wa BancABC Tanzania (kulia) akimkabidhi msaada wa vyakula mbali mbali Mkurugenzi wa Kituo cha Watoto yatima cha New Faraja kilichopo Mburahati Jijini Dar es Salaam. BancABC Tanzania ambayo ni kampuni tanzu ya Atlas Mara ilitoa msaada wa vyakula mbalimbali pamoja na kuandaa futari kwa watoto waliopo kwenye kituo hicho kama ishara ya kuonyesha upendo kwenye kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadan.

Na. Damian Kunambi, Njombe

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva akiambatana na Mkurugenzi wa Halamashauri, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wananchi wilayani humo wamefanya Dua/Kisomo Maalum cha kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili azidi kupata kheri, hekmana baraka.

Akizungumza mara baada ya kufanyika kisomo hicho katika msikiti wa Wilaya ya Ludewa mkuu huyo wa wilaya amesema Rais Dkt. Samia amekuwa ni kiongozi anaye liongoza vyema Taifa la Tanzania hivyo anapopata baraka taifa zima linapata baraka pia kupitia yeye.

"Rais wetu amekuwa ni kiongozi bora na mwenye hekma, hivyo hatuna budi kumwombea kwa Mungu ili aweze kuendeleza ubora alio nao na kile ambacho Mungu amekiweka ndani yake".

Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya hiyo Sunday Deogratius amempongeza mkuu huyo wa Wilaya kwa kuandaa kisomo hicho kilicho ambatana na futari na kuongeza kuwa Rais Dkt. Samia amefanya maendeleo makubwa katika halmashauri mbalimbali ikiwemo halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ambayo imepiga hatua kwenye maendeleo ya elimu, afya, miundombinu ya barabara na sekta nyinginezo.

Aidha kwa upande wake shekhe wa Wilaya hiyo Haruna Rahim amemshukuru mkuu wa wilaya kwa kuwaunganisha katika kufanya kisomo hicho pamoja na kupata futari kwani kwa kufanya hivyo kunaongeza Swawabu kutoka kwa mwenyezi Mungu na hasa katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan.

Kisomo hicho cha kumwombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kiliambatana na Iftari iliyo andaliwa na mkuu huyo wa Wilaya Victoria Mwanziva katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo ambapo waumini wote wa kiislamu na wageni waalikwa walijuika pamoja kupata ftari hiyo.

Sanjari na kisomo hicho na futari lakini pia mkuu huyo wa Wilaya alimkabidhi Shekhe Haruna zawadi ya pikipiki aina ya King lion 150 yenye thamani ya shilingi 2,600,000 milion ili iweze kumsaidia katika mizunguko yake mbalimbali huku mbunge wa jimbo la Ludewa akitoa hundi ya shilingi 1,000,000 kwaajili ya ujenzi wa msikiti.









Top News